Takribani watu 11 wamefariki dunia na wengine 14 kujeruhiwa baada ya tukio la ufyatuaji risasi lililotokea mapema Jumamosi asubuhi Afrika Kusini. Tukio hilo limesababisha mauaji jijini Pretoria.
Kwa mujibu wa polisi, tukio hilo lilitokea majira ya saa 4:00 asubuhi katika hosteli ya Saulsville, iliyopo Atteridgeville, magharibi mwa Pretoria.
Miongoni mwa waliopoteza maisha ni watoto watatu. Polisi wamedhibitisha kuwa mvulana wa miaka mitatu alifariki, pamoja na mvulana wa miaka 12 na msichana wa miaka 16.
Walioumia walikimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu. Hadi sasa, hakuna taarifa kamili kuhusu hali zao au iwapo kuna waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Maafisa wa usalama wamesema uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha tukio na wahusika waliotekeleza shambulizi hilo.
Afrika Kusini ina historia ya muda mrefu ya matukio ya uhalifu unaohusiana na silaha za moto. Nchi hiyo pia ina mojawapo ya viwango vya juu zaidi vya mauaji duniani, kwa mujibu wa takwimu za usalama.
Tukio hili limeongeza wasiwasi kuhusu usalama wa raia, hasa katika maeneo ya makazi yenye watu wengi. Mauaji na uhalifu si jambo geni Pretoria na Afrika Kusini kiujumla.


