Utangulizi
Mahusiano kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini yamekuwa yakiyumba kwa zaidi ya miaka 70 — mara yakiwa ya mashaka, mara yakiwa na matumaini. Tangu vita ya Korea (1950–1953) ilipomalizika bila mkataba wa amani rasmi, nchi hizi mbili zimeendelea kuishi kwa tahadhari ya kijeshi na mashindano ya propaganda. Hivi karibuni, Korea Kusini imezima spika zake za propaganda, kwa kufuata maelekezo ya raisi wake mpya Lee Jae-myung, hatua inayotafsiriwa na wachambuzi kama ishara ya kutafuta mwelekeo mpya wa mawasiliano.
1. Historia Fupi ya Migogoro
Baada ya Vita ya Pili ya Dunia, Korea iligawanywa katika maeneo mawili: kaskazini (chini ya ushawishi wa Soviet) na kusini (chini ya Marekani). Mwaka 1950, Korea Kaskazini ilivamia Kusini, na vita ya miaka mitatu ilifuata. Mkataba wa kusitisha vita ulisainiwa mwaka 1953, lakini amani ya kudumu haijawahi kufikiwa.
Tangu hapo:
- Kila upande umetafuta uhalali wa kisiasa kupitia propaganda.
- Majaribio ya nyuklia kutoka Pyongyang yamekuwa chanzo kikubwa cha wasiwasi.
- Vikao vya mazungumzo vimekuwepo lakini vimekuwa vikitawaliwa na sintofahamu ya mara kwa mara.
2. Spika za Propaganda: Silaha za Maneno
Moja ya alama ya mivutano ya kisiasa kati ya nchi hizi ni matumizi ya spika kubwa kwenye mpaka — hasa Panmunjom au DMZ (Demilitarized Zone). Korea Kusini huzitumia kutangaza muziki wa K-pop, matangazo ya kisiasa, na taarifa za hali ya maisha Kusini. Kaskazini, kwa upande wake, hutangaza ujumbe wa kulaani viongozi wa Kusini na Marekani, mara nyingine kwa sauti ya hasira au muziki wa kijeshi.

Mwezi Juni 2024, Korea Kaskazini ilifufua spika zake kufuatia kile ilichokiita “harakati mpya katika uongozi wa Seoul.” Hali hii ilitokana na Korea Kaskazini imekuwa ikituma maputo makubwa yaliyojaa taka kama plastiki na kinyesi cha wanyama kuelekea Kusini. Tangu Mei, zaidi ya maputo 1,000 yameripotiwa kutua maeneo ya mpaka.
3. Rais Mpya wa Korea Kusini: Je, amekuja na Mabadiliko au Kuimarisha Msimamo?
Korea Kusini ilimchagua Rais mpya katika uchaguzi wa Mei 2025: Lee Jae-Myung, mwanasiasa mwenye msimamo tulivu dhidi ya Kaskazini, lakini anayesisitiza “usalama wa kikanda na ushirikiano wa kimataifa.”

Baadhi ya maelezo ya awali ya sera yake:
- Kudumisha uhusiano wa karibu na kurudisha imani ya wananchi wa Korea Kusini kwa serikali.
- Kuweka wazi kuwa Korea Kusini haitakubali “vitisho vya sauti” kutoka Pyongyang.
- Kupendekeza mazungumzo ya kiusalama kupitia ASEAN au Umoja wa Mataifa badala ya mazungumzo ya pande mbili pekee.
Rais Yoon aliondolewa madarakani mwanzo wa mwezi April, 2025 kwa kufunguliwa mashitaka ya ukiukaji wa katiba, baada ya kuiweka Korea Kusini chini ya hali ya hatari ya kijeshi kwa muda mfupi mwezi Desemba, akidai kuwa kulikuwa na vitisho kutoka kwa maadui wa taifa na watu wanaoiunga mkono Korea Kaskazini.
4. Wito wa Dunia na Majibu ya Jumuiya ya Kimataifa
- Marekani imeahidi kuendelea kulinda Korea Kusini kwa njia za kijeshi na kisiasa.
- China inasisitiza utulivu wa eneo na inahimiza majadiliano.
- Umoja wa Mataifa umetaka pande zote kuacha uchokozi wa maneno na kurejea kwenye meza ya mazungumzo.
5. Tunajifunza Nini?
Mzozo huu unaonesha jinsi teknolojia rahisi kama spika inaweza kubeba uzito wa mgogoro wa kimataifa. Pia, unadhihirisha kuwa uchaguzi wa ndani wa nchi moja unaweza kuleta athari za mbali, hata hadi kwenye mipaka ya kijeshi.
Katika dunia ya leo, sauti siyo tu njia ya mawasiliano, bali ni silaha ya kisiasa.
Hitimisho
Historia ya Korea Kaskazini na Kusini ni hadithi ya taifa moja lililopasuliwa na siasa za enzi ya Vita Baridi. Rais mpya wa Korea Kusini anaingia madarakani wakati ambapo hali ya mpaka imetulia tena — si kwa risasi, na si kwa maneno yanayotangazwa kwa spika. Swali linalobaki: Je, mazingira haya yatachochea amani, umoja na ushirikiano?


